MSANII nyota wa filamu nchini,
Steven Kanumba amefariki dunia kutokana na tatizo la mtikisiko wa ubongo
linalojulikana kitalaamu kama Brain
Concussion, taarifa za kitabibu zimeeleza.
Taarifa hizo za ndani,
zilizopatikana jana baada ya jopo la madaktari bingwa watano wa Hospitali ya
Taifa Muhimbili kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu huyo, zimeeleza kuwa
tatizo hilo
linaweza kumfanya mtu apoteze maisha mara moja au baada ya siku kadhaa. Mmoja
wa madaktari hao ambaye aliomba jina lake
lisitajwe gazetini alisema waligundua
tatizo hilo
baada ya kumfanyia uchunguzi huo kwa zaidi ya saa mbili.
“Tulianza kuufanyia uchunguzi
mwili wa marehemu kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 6:45 mchana na tukagundua
kuwa marehemu alifariki kutokana na mtikisiko wa ubongo kwa kitaalamu, Brain
Concussion,” alisema daktari huyo. Alisema Kanumba alipata mtikisiko wa ubongo
ambao husababisha kufeli kwa mfumo wa upumuaji (cardio-respiratory failure)
“Kilichomuua hasa ni mtikisiko wa ubongo, ambao endapo unatokea katika sehemu
ya nyuma ya ubongo (cerebrum), huua kwa haraka” alisema daktari huyo na kuongeza
kuwa mtikisiko wa ubongo wa nyuma, husababisha matatizo ya mfumo wa
upumuaji na hilo limeonekana katika mwili wake.
“Baada ya ubongo wake kutikiswa
kwa nguvu, mfumo wa upumuaji ulifeli na ndiyo maana tumekuta kucha za Kanumba
zikiwa na rangi ya bluu, huku mapafu yake yakiwa yamevilia damu na kubadilika
kuwa kama maini, hizo ndizo dalili za kufeli
kwa mfumo wa upumuaji.”
“Mtu aliyepata mtikisiko wa ubongo
huweza kutokwa na mapovu mdomoni na hukoroma kabla ya kukata roho na ndivyo
ilivyokuwa kwa Kanumba kabla hajafariki.”
Daktari mwingine aliyeshiriki
katika uchunguzi huo ambaye pia aliomba jina lake lisitajwe
alisema ubongo wa mwigizaji huyo ulikuwa umevimba na kushuka karibu na uti wa
mgongo na hivyo kuathiri mfumo wa upumuaji.
Alisema sehemu ya maini na
majimaji ya machoni ya marehemu, vimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili
kubaini endapo kuna sumu au kitu kingine katika mwili huo.
Baba mzazi azungumza Baba mzazi wa
mwigizaji huyo, Charles Musekwa Kanumba alisema kwamba alipata taarifa za kifo
cha mwanawe Jumamosi saa 10:00 alfajiri baada ya kupigiwa simu na dada wa
marehemu, Sara Kanumba. “Sara aliniuliza: ‘Una taarifa yoyote kuhusu
mwanao Kanumba?’ Nikamjibu kuwa sina taarifa yoyote, ndipo aliponieleza habari
za kifo hicho. Aliniambia Kanumba hatupo naye tena amefariki kwa kuanguka,
amekorofishana na mpenzi wake.” alisema taarifa hizo zilimsababisha
aishiwe nguvu kwa kuwa kilikuwa kifo cha ghafla… “Basi kuanzia hapo, nilianza
kupigiwa simu za kupewa pole, ndipo nilipoamini kumbe mwanangu amefariki.”
Akizungumzia kuchelewa
kufika msibani, alisema kumetokana na tatizo la mawasiliano. Awali, alikuwa
amepanga mtoto wake Kanumba akazikiwe Mwanza kwa babu yake ndiyo maana hakufika
mapema msibani. “Nilikuwa nimepanga apitishwe hapa kwangu Shinyanga
aagwe, halafu tumpeleke Mwanza kwa babu yake kumzika huko lakini alipokuja mama
yake alinishauri kuwa huko kutakuwa na nafasi ndogo kwa sababu watu ni wengi
pia alikuwa na marafiki wengi, wengine wa kutoka nje ya nchi kwa hiyo alinishawishi
na tukakubaliana kumzika Dar es Salaam,” alisema.
Pia alikanusha uvumi kuwa hajafika
msibani kwa kuwa walikuwa na ugomvi na marehemu akisema walishamaliza tofauti
zao. Alisema anatarajia kufika leo usiku tayari kushiriki mazishi hayo.
Wabunge kilio Jana, baadhi
ya wabunge waliofika nyumbani kwa marehemu Kanumba waliangua vilio wakati
walipotoa salamu zao za rambirambi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Martha
Mlata hakuzungumza na badala yake aliimba kipande cha wimbo uliozungumzia kifo
na maneno ya wimbo huo yalionekana kuwagusa wafiwa na kusababisha vilio kuanza
upya huku baadhi wakipoteza fahamu.
Mbunge mwingine, Neema Mwinyimgaya
aliongeza majonzi masibani hapo alipounganisha msiba huo na wa mama yake… “Mama
yangu amefariki miezi mitatu iliyopita, huko uliko mama, nakuomba umpokee
kijana mwenzetu,” alisema mbunge huyo na kushindwa kuendelea.
Wabunge wengine waliohudhuria
msiba huo ni Ismail Aden Rage (Tabora Mjini), Aboud Juma (Kibaha Vijijini),
Mussa Azan Zungu (Ilala), Abbas Mtemvu (Temeke), Peter Serukamba (Kigoma Mjini)
na Ritha Kabati (Viti Maalumu).
Kova na mchango wa Kanumba
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema
anakumbuka mchango wa Kanumba katika kuzuia uhalifu jijini.
“Tulishirikiana naye pamoja na
wasanii wengine kuandaa bonanza maalumu ambalo lilidhamiria kukabiliana na
uhalifu hapa jijini na kwa kweli mchakato ule ulifanikiwa kwani uhalifu
ulipungua kwa kiasi kikubwa” alisema Kova.
“Kifo chake kimekuwa cha ghafla
mno na nafikiri kujiweka tayari (kiimani) ni jambo ambalo kila mmoja anatakiwa
kuwa makini nalo katika maisha yake,” alisema Kova.
Ratiba ya mazishi
2:30 - Msafara kutoka Hospitali ya
Taifa Muhimbili kupitia Barabara ya Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi
Viwanja vya Leaders Club.
3:30 - Misa ya kumuombea na salamu
mbalimbali.
6:00 – Kuaga
9:00 - Kuelekea Makaburi ya
Kinondoni kupitia Barabara ya Tunisia
Habari kwa hisani ya Gazeti la
Mwananchi
No comments:
Post a Comment